Katika kipindi cha miezi mitatu, kuanzia Agosti hadi Novemba 2024, TIBA kwa msaada wa Women Fund Tanzania (WFT), ilitekeleza mradi wa kuondoa ukatili wa kijinsia katika masoko na maeneo ya biashara ya wazi. Mradi huu uliwaleta pamoja wanawake wakulima na wauza mbogamboga ili kujadili changamoto wanazokutana nazo, kupata elimu kuhusu haki zao, na kubuni mikakati ya kujilinda dhidi ya mifumo kandamizi inayowakandamiza katika sekta ya biashara ndogondogo. Kupitia warsha na mikutano ya DADA GENGE Hub, wanawake walipata nafasi ya kushiriki mijadala, kusimulia changamoto zao, na kushirikishana mbinu za kukabiliana na rushwa ya ngono na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia. Mnamo tarehe 15 Agosti 2024, warsha ya kwanza ilifanyika katika hoteli ya JAMIREX, Mwenge, ikihusisha washiriki 40 waliopatiwa mafunzo kuhusu haki za wanawake na mbinu za kupambana na ukatili wa kijinsia. Mafanikio ya warsha hii yalijumuisha kuundwa kwa Muongozo wa Jinsia na Haki za Wanawake kwa masoko na maeneo ya biashara, pamoja na kutambuliwa kwa vinara 25 wa kupinga ukatili wa kijinsia, ambao walipewa jukumu la kukusanya kesi na kuripoti matukio ya unyanyasaji. Tarehe 29 Agosti 2024, DADA GENGE Hub ilitoa elimu kuhusu rushwa ya ngono, huku washiriki wakishiriki ushuhuda wa changamoto wanazopitia na kuunda nyimbo za hamasa dhidi ya ukatili wa kijinsia. Aidha, tarehe 26 Septemba 2024, mkutano mwingine wa DADA GENGE Hub ulifanyika, ambapo wanawake walijifunza namna ya kutumia mifumo ya kidigitali kupata masoko na kuongeza thamani ya biashara zao, hali iliyosaidia wengi wao kuachana na kausha damu na badala yake kuwekeza katika vikundi vyao vya VICCOBA. Hatimaye, tarehe 5 Novemba 2024, mkutano wa mwisho wa DADA GENGE Hub ulihusu ukusanyaji wa taarifa za mwisho za mradi, ambapo wanawake walitoa ushuhuda wa mafanikio, ikiwa ni pamoja na kupachika Muongozo wa Jinsia katika maeneo yao ya biashara. Mradi huu umeleta mabadiliko makubwa, ukifanikisha kutoa elimu kwa wanawake 113 kuhusu haki zao, msaada wa kisheria, na namna ya kuripoti ukatili wa kijinsia, huku zaidi ya wanawake 113 wakipata elimu kuhusu rushwa ya ngono. Kwa mafanikio haya, Kijiwe cha Mbogamboga kimekuwa sehemu muhimu ya kuhamasisha haki na usawa kwa wanawake katika sekta ya biashara ya masokoni na magengeni.